Tunabadili Masharti ya Huduma na Sera yetu ya Faragha zinazohusiana na utumaji ujumbe kati ya biashara na wateja wao kwenye WhatsApp. Pia tunatoa maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyokusanya, kushiriki na kutumia data.
Ahadi yetu ya kulinda faragha yako haibadiliki. Mawasiliano yako ya binafsi bado yanalindwa kwa ufumbaji wa mwisho hadi mwisho, hii ina maana kwamba hakuna mtu nje ya soga zako, ikiwa ni pamoja na WhatsApp au Facebook, anaweza kuyasoma au kuyasikiliza.
Ni jukumu letu kufafanua masasisho haya kwa uwazi. Haya ndiyo baadhi ya mambo unayofaa kuyajua:
Kila siku, mamilioni ya watu hutumia WhatsApp kuwasiliana na biashara, ziwe kubwa au ndogo. Unaweza kuwasiliana na biashara ili kuuliza maswali, kununua au kupata taarifa. Ni wewe unayeamua kama unataka kupiga soga na biashara kwenye WhatsApp, unaweza kuzizuia au kuziondoa kwenye orodha yako ya waasiliani.
Biashara kubwa, kama vile mashirika ya ndege au maduka makubwa, yanaweza kupokea maelfu ya mawasiliano kutoka kwa wateja wao kwa wakati mmoja - wakiomba taarifa kuhusu ndege au kufuatilia bidhaa waliyoagiza. Ili kuhakikisha kwamba majibu yanatolewa haraka, biashara hizi zinaweza kutumia Facebook kuwa mtoa huduma za teknolojia ya kudhibiti baadhi ya majibu kwa niaba yao. Tutaweka alama waziwazi kwenye soga ili ufahamu hali hii inapotokea.
Mabadiliko kwenye Sera yetu ya Faragha yanakupa maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyodhibiti taarifa zako. Tumeongeza maelezo zaidi kwenye baadhi ya sehemu za Sara yetu ya Faragha na pia tumeongeza sehemu mpya. Pia tumerahisisha mpangilio wa Sera ya Faragha na kurahisisha utumiaji na usogezaji.
Unaweza kupakua ripoti ya taarifa na mipangilio ya akaunti yako ya WhatsApp hapa.
WhatsApp wala Facebook haziwezi kuona maudhui unayoshiriki na familia na marafiki zako, hayo ni pamoja na ujumbe na simu, viambatisho mnavyotumiana au unaposhiriki mahali ulipo. Hatuweki kumbukumbu ya watu wowote wanaotumiwa ujumbe au kupigiwa simu na WhatsApp haishiriki waasiliani wako na Facebook.
WhatsApp haiwezi kuipa biashara nambari yako, pia sera zetu zinakataza biashara kuwasiliana na wewe kwenye WhatsApp kabla ya kupokea idhini yako kufanya hivyo.
Vipengele vyetu vya ziada vya faragha, kama vile kufanya ujumbe wako utoweke au kudhibiti anayeweza kukuongeza kwenye vikundi, hukupa safu ya ziada ya faragha.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali hakiki masharti na sera yetu ya faragha. Pia unaweza kupata majibu ya maswali yanayoulizwa mara kwa mara hapa.