Hivi karibuni tulisasisha Sera yetu ya Faragha na tumepokea maswali mengi yenye umakinifu. Kwa sababu ya uvumi unaosambazwa, tungependa kujibu baadhi ya maswali yanayoulizwa sana ambayo tumeyapokea. Huwa tunajitahidi sana kubuni WhatsApp kwa namna inayowasaidia watu kuwasiliana kwa faragha.
Tunapenda kubainisha waziwazi kwamba sasisho hili la sera haliathiri faragha ya ujumbe mnaotumiana na marafiki au familia kwa namna yoyote ile. Mabadiliko haya yanahusu vipengele vya hiari vya biashara kwenye WhatsApp na yanatoa ufafanuzi zaidi kuhusu jinsi tunavyokusanya na kutumia data. Pata maelezo zaidi kuhusu vipengele vipya vya biashara na sasisho la Sera ya Faragha ya WhatsApp hapa.
Hatuwezi kusoma ujumbe au kusikiliza simu zako za binafsi, nao Facebook pia hawawezi: WhatsApp wala Facebook haziwezi kusoma ujumbe au kusikiliza simu kati yako na marafiki, familia na wafanyakazi wenza mnapotumia WhatsApp. Chochote mnachoshiriki, hubakia kati yenu. Hii ni kwa sababu ujumbe wako wa binafsi hulindwa kwa ufumbaji wa mwisho hadi mwisho. Hatutawahi kamwe kudhoofisha ulinzi huu na huwa tunabainisha kwenye kila soga ili ufahamu kujitolea kwetu. Pata maelezo zaidi kuhusu usalama wa WhatsApp hapa.
Hatuhifadhi kumbukumbu za kila mtu anayetumiwa ujumbe au kupigiwa simu kwenye WhatsApp: Ingawa kwa kawaida watoa huduma na waendeshaji wa mitandao ya simu za mikononi huhifadhi taarifa hizi, tunaamini kwamba kuhifadhi rekodi hizi kwa watumiaji bilioni mbili kunaweza kuwa hatari ya faragha na usalama kwa hivyo hatuzihifadhi.
Hatuwezi kuona mahali unapopashiriki, Facebook pia haiwezi: Unaposhiriki mahali ulipo na mtu kwenye WhatsApp, taarifa zako za mahali hulindwa kwa ufumbaji wa mwisho hadi mwisho, kumaanisha kwamba hakuna mtu mwingine anaweza kuona mahali ulipopashiriki isipokuwa watu ulioshiriki nao.
Hatushiriki waasiliani wako na Facebook: Ukituruhusu, tunaweza tu kufikia nambari za simu zilizo kwenye kitabu cha anwani cha simu yako ili kurahisisha na kufanya mawasiliano yawe ya uhakika zaidi, hatushiriki orodha yako ya waasiliani na programu nyingine zinazotolewa na Facebook.
Vikundi vitasalia kuwa vya faragha: Tunatumia uwanachama wa vikundi kuwasilisha ujumbe na kulinda huduma yetu dhidi ya barua taka na matumizi mabaya. Hatushiriki taarifa hizi na Facebook kwa madhumini ya matangazo. Isitoshe, soga hizi za binafsi zimefumbwa mwisho hadi mwisho kwa hivyo hatuwezi kuziona.
Unaweza kufanya ujumbe utoweke: Kwa faragha ya ziada, unaweza kuchagua kufanya ujumbe wako utoweke kwenye soga baada ya kuutuma. Pata maelezo zaidi kuhusu hili kwenye makala haya ya Kituo cha Msaada.
Unaweza kupakua data yako: Unaweza kupakua na kuona taarifa tulizonazo kwenye akaunti yako moja kwa moja kutoka kwenye programu. Pata maelezo zaidi kuhusu hili kwenye makala haya ya Kituo cha Msaada.
Kila siku, mamilioni ya watu kote duniani huwasiliana na biashara za ukubwa mbalimbali kwa njia salama kwenye WhatsApp. Tunataka kuboresha na kurahisisha mawasiliano haya ukichagua kuwasiliana na biashara. Tutakuwa tukibainisha kwenye WhatsApp kila wakati unapowasiliana na biashara yoyote inayotumia vipengele hivi.
Huduma za Facebook za upangishaji: Mawasiliano kati yako na biashara huwa tofauti na unapowasiliana na marafiki au familia. Baadhi ya biashara kubwa huhitaji huduma za kupangisha ili kudhibiti mawasiliano yao. Ndiyo maana tunazipa biashara chaguo la kutumia huduma salama za upangishaji zinazotolewa na Facebook ili ziweze kudhibiti soga za WhatsApp na wateja wao, kujibu maswali, na kutuma taarifa muhimu kama vile stakabadhi za ununuzi. Lakini wakati wowote unapowasiliana na biashara kupitia simu, barua pepe, au WhatsApp, inaweza kuona unachosema na huenda ikatumia taarifa hizo kwa madhumuni yake ya mauzo, ambayo yanaweza kujumuisha kutangaza kwenye Facebook. Ili kuhakikisha kwamba unafahamu, tunabainisha kwa uwazi ukiwa unafanya mazungumzo na biashara ambayo imechagua kutumia huduma za upangishaji zinazotolewa na Facebook.
Kugundua biashara: Unaweza kuona tangazo kwenye Facebook lililo na kitufe cha kutumia biashara ujumbe kwa kutumia WhatsApp. Ikiwa una WhatsApp kwenye simu yako, utakuwa na chaguo la kuitumia biashara hiyo ujumbe. Facebook inaweza kutumia ufahamu wa unavyoingiliana na matangazo haya ili kubinafsisha matangazo unayoona kwenye Facebook.
Malipo kwenye WhatsApp: Malipo ya WhatsApp yanayowezeshwa na UPI yanasimamiwa na sera tofauti ya faragha unayoweza kuipata hapa, sera hiyo ya faragha haiathiriwi na sasisho hili.