Jinsi WhatsApp Inavyosaidia Kukabili Unyanyasaji wa Watoto
WhatsApp haikubali kabisa dhuluma za kingono na unyanyasaji dhidi ya watoto na tunawapiga marufuku watumiaji tukifahamu kwamba wanahusika katika kushiriki maudhui yanayonyanyasa au kuhatarisha watoto. Pia tunaripoti maudhui na akaunti zinazokiuka kwa Kituo cha Taifa cha Watoto Waliopotea na Wanaonyanyaswa (NCMEC), ambacho huelekeza vidokezo hivi vya mtandaoni kwa Vyombo vya Kutekeleza Sheria kote duniani. Tuna vipengele na vidhibiti ambavyo husaidia kuzuia unyanyasaji na dhuluma, pia tumeajiri timu kakamavu inayojumuisha wajuzi wa utekelezaji wa sheria, sera za usalama mtandaoni, wachunguzi na wale wa ukuaji wa teknolojia ili waongoze juhudi hizi.
Kuzuia Matumizi Mabaya
WhatsApp iliundwa kwa ajili ya mawasiliano ya binafsi. Ili kulinda faragha na usalama wa watumiaji wetu, tunatumia ufumbaji wa mwisho hadi mwisho kwa chaguomsingi, hii ina maana kwamba mtumaji na mpokeaji pekee ndio wanaoweza kuona yaliyo kwenye ujumbe. Ili kudumisha usalama wa watumiaji wetu, tunajituma kuzuia matukio ya matumizi mabaya kabla hayajatokea. Tofauti na maeneo ya umma, katika WhatsApp huwezi kutafuta watu usiowajua. Unahitaji nambari ya simu ya mtu ili uweze kuwasiliana naye, mara ya kwanza unapopokea ujumbe kutoka kwa mtu asiye kwenye kitabu chako cha anwani, tunakuuliza ikiwa unataka kumzuia au kumripoti. Asilimia 90 ya ujumbe unaotumwa kwenye WhatsApp huwa kati ya watu wawili na ukubwa wastani wa kikundi ni chini ya watu 10. Tunawapa watumiaji uwezo wa kuamua ni nani anaweza kuwaongeza kwenye vikundi na pia tunadhibiti idadi ya soga ambapo unaweza kusambaza ujumbe kwa wakati mmoja ili kudhibiti usambaaji wa maudhui hatari.
Pia tunashirikiana na watoa huduma za duka za programu ili kuzuia ueneaji wa programu zilizo na taswira zinazowanyanyasa watoto (CEI) au zinazojaribu kuunganisha watu wanaovutiwa na kushiriki aina hii ya maudhui kupitia viungo vya kualikana. Tunazuia injini maarufu za utafutaji kuorodhesha viungo vya mialiko.
Utambuaji
Ili kukabili zaidi dhuluma za kingono dhidi ya watoto, WhatsApp hutegemea taarifa zote ambazo hazijafumbwa, ikiwa ni pamoja na ripoti zinazopigwa na watumiaji, ili kutambua na kuzuia aina hizi za utumiaji mbaya. Tunaendelea kuboresha teknolojia yetu ya utambuaji kila wakati.
Mbinu zetu za utambuaji zinajumuisha utumiaji wa teknolojia ya ngazi ya juu, ikiwemo zile za kulinganisha picha na video, ili kuchanganua taarifa ambazo hazijafumbwa kama vile picha za jalada na vikundi na ripoti zinazotolewa na watumiaji ili kubaini uwepo wa taswira zinazojulikana za kuwanyanyasa watoto. Tuna teknolojia ya ziada ya kutambua taswira mpya zisizojulikana zinazowanyanyasa watoto, zilizo miongoni mwa taarifa ambazo hazijafumbwa. Pia tunatumia viainishaji vya mfumo wa mashine kujifunza ili kuchanganua maandishi yaliyo katika sehemu kama vile jalada za watumiaji na maelezo ya vikundi na vilevile kuhakiki maelezo ya vikundi ili kutambua kama kuna maudhui yanayoshukiwa kuwa ni taswira zinazowanyanyasa watoto.
Pamoja na juhudi zetu za kuwa mbele kutambua, WhatsApp huwahizima watumiaji kuripoti kwetu maudhui yanayotatiza. Watumiaji pia wanaweza kuzuia au kuripoti akaunti ya mtu binafsi au kikundi wakati wowote. Pata maelezo zaidi kuhusu kuwa salama kwenye WhatsApp katika Kituo Chetu cha Msaada.
Kwa kutumia mikakati hii, WhatsApp hupiga marufuku zaidi ya akaunti 300,000 kwa mwezi kwa kushukiwa kushiriki taswira zinazowanyanyasa watoto.
Kushirikiana na Watekelezaji wa Sheria
WhatsApp inatambua kazi inayofanywa na watekelezaji wa sheria ili kuhakikisha usalama wa watu kote duniani. Tunatagusana na watekelezaji wa sheria mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba wanajua jinsi ya kuwasliniana nasi na wanaelewa jinsi ya kuomba jambo kutoka WhatsApp. Kituo chetu cha Taarifa Kwa Ajili ya Watekelezaji wa Sheria kina mfumo wa mtandaoni kinachowezesha watekelezaji wa sheria kutuma maombi haya ya kisheria kwa njia salama.
WhatsApp ikifahamu kwamba kuna taswira zinazowanyanyasa watoto kwenye mfumo wetu, huwa tunapiga marufuku akaunti zinazohusika. Pia tunaondoa taswira hizo na kuziripoti pamoja na maelezo ya akaunti husika katika Kituo cha Kitaifa cha Watoto Waliopotea na Wanaonyanyaswa (NCMEC) kwa mujibu wa sheria za Marekani.
NCMEC ikielekeza masuala hayo kwa watekelezaji wa sheria ili yachunguzwe, WhatsApp huwa tayari kujibu maombi halali ya watekelezaji wa sheria inavyotakiwa. WhatsApp imepokea majibu kutoka kwa watekelezaji wa sheria kwamba juhudi zetu zimesaidia kuwaokoa waathiriwa wa unyanyasaji wa watoto.
Februari, 2021 (Takwimu za akaunti zilizopigwa marufuku ni kwa mujibu wa uchanganuzi wa robo ya nne ya 2020)