Kuanzisha Jumuiya Salama na za Faragha kwenye WhatsApp

Tunaanzisha kipengele cha Jumuiya kwenye WhatsApp kwa ajili ya vikundi mahususi vinavyohitaji zana zaidi ili kupanga na kudhibiti mazungumzo yao. Kwa kawaida, aina hizi za vikundi huwa na uhusiano ambapo watu wanafahamiana na wanatekeleza mambo pamoja au wanavutiwa na kitu fulani mahususi.
Wazazi shuleni, vikundi vya kieneo, na hata wafanyakazi katika ofisi ndogo sasa wanategemea WhatsApp kama njia yao kuu ya mawasiliano. Vikundi hivi vinahitaji njia za kuwasiliana kwa faragha ambazo ni tofauti na mitandao ya kijamii lakini zinazojumuisha zana zaidi za kuwezesha mazungumzo ya moja kwa moja badala ya kutumia barua pepe au matangazo.
Vigezo muhimu kwa kila Jumuiya kwenye WhatsApp ni maelezo na menyu ya vikundi ambavyo watu wanaweza kujiunga. Vigezo hivi hutoa muundo na mpangilio kwa mazungumzo ya vikundi vikubwa vya mseto, unaowawezesha watu kuzingatia suala muhimu kwao. Tunasanidi masasisho kadhaa ili kutoa njia salama na za faragha kwa vikundi hivi kuwasiliana kwenye WhatsApp tukitumia kanuni zifuatazo kama mwongozo wetu.
Idhini zaidi kwa wasimamizi
Tunaunda zana mpya zitakazowawezesha wasimamizi kudhibiti mazungumzo katika vikundi vyao vya faragha. Wasimamizi wana jukumu la kuanzisha na kudhibiti Jumuiya kwenye WhatsApp. Msimamizi anaweza kuchagua vikundi atakavyojumuishwa kwenye Jumuiya yake kwa kuanzisha vikundi vipya au kwa kuunganisha vikundi ambavyo tayari vipo. Wasimamizi wa jumuiya pia watakuwa na idhini ya kuondoa vikundi kwenye Jumuiya na kuwaondoa wanakikundi kwenye Jumuiya. Pia, wasimamizi wa kikundi wataweza kufuta soga au maudhui ya matusi yasiyowafaa wanakikundi. Tutawapa wasimamizi nyenzo kuhusu jinsi ya kutumia vipengele hivi vipya.
Idhini zaidi kwa watumiaji ili kuwawezesha kudhibiti soga zao
Kando na kutoa zana mpya kwa wasimamizi, watumiaji wanaweza kudhibiti mawasiliano yao kwenye Jumuiya. Mipangilio yetu iliyopo inawawezesha watumiaji kubainisha ni nani anayeweza kuwaongeza kwenye kikundi - mipangilio hii itatumika pia kwa Jumuiya. Watumiaji pia wataweza kuripoti matumizi mabaya, kuzuia akaunti za watumiaji, na kuondoka kwa urahisi kwenye Jumuiya ambazo hawangependa kushiriki tena. Pia, tunaongeza kipengele cha kuondoka kwenye kikundi kimyakimya, ili walio kwenye kikundi wasiarifiwe mtu anapoamua kuondoka.
Marekebisho ya Ukubwa, Upatikanaji, na Usambazaji wa Ujumbe
Japo programu zingine hutoa soga za vikundi bila vikwazo, WhatsApp inaelekeza mchakato wa uundaji wa bidhaa zetu uwe wenye kukidhi mahitaji ya mashirika na vikundi vingine ambapo watu wengi tayari wanajuana. Tofauti na mitandao ya kijamii na huduma zingine za kutuma ujumbe, WhatsApp haitajumuisha kipengele cha kutafuta au kugundua Jumuiya mpya kwenye huduma yetu.
Ili kudhibiti ujumbe, wasimamizi wa Jumuiya pekee ndio wataweza kutuma ujumbe kwa Wanajumuiya wote - hii inajulikana kama kikundi cha matangazo kwa jumuiya. Mwanzoni huduma ya matangazo kwa jumuiya itapatikana kwa maelfu ya watumiaji. Wanajumuiya wanaweza kupiga soga katika vikundi vidogo ambavyo wasimamizi wameanzisha au kuidhinisha. Tutaongeza ukubwa wa vikundi hatua kwa hatua kadiri tunavyotoa vidhibiti zaidi kwa wasimamizi na watumiaji.
Tutaendelea kudhibiti usambazaji wa ujumbe kwenye WhatsApp ili mazungumzo yawe ya faragha. Kutokana na kuanzishwa kwa Jumuiya, jumbe ambazo tayari zimesambazwa zitaweza tu kutumwa kwa kikundi kimoja kwa wakati mmoja, badala ya vitano, kama ilivyo kwenye vikwazo vya sasa vya usambazaji. Tunaamini kuwa hii itapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kueneza taarifa potovu kwenye vikundi vya jumuiya.
Ufumbaji wa Mwisho hadi Mwisho na Faragha ya Nambari ya Simu
Kutokana na hali ya faragha ya soga kwenye jumuiya hizi za watu wanaowasiliana sana, WhatsApp itaendelea kulinda ujumbe kupitia ufumbaji wa mwisho hadi mwisho ili uonekane na watumiaji wa vikundi husika pekee. Teknolojia hii ya usalama hulinda mazungumzo nyeti kati ya mashirika, wafanyakazi na vikundi vya kibinafsi.
Ili kulinda faragha ya watumiaji, nambari yako ya simu itafichwa kwenye Jumuiya na itaonekana tu na wasimamizi wa Jumuiya na wengine mlio nao katika kikundi kimoja. Hii itasaidia kuzuia mawasiliano yasiyotakikana na pia itapunguza hatari ya kupata nambari za simu za watu.
Kuchukulia hatua Jumuiya zinazoruhusu maudhui yasiyofaa
Hatua na vidhibiti hivi vipya vimeundwa ili kuwawezesha wasimamizi wa Jumuiya kushughulikia matatizo katika vikundi vyao, kwa kuwa wanavifahamu vyema. Tutaendelea pia kuwahimiza watumiaji waripoti kwetu ujumbe na Jumuiya zinazokiuka masharti.
Itakaporipotiwa kwetu kuhusu Jumuiya zinazojihusisha na matumizi mabaya kama vile kusambaza maudhui ya unyanyasaji wa watoto kingono, au kupanga vurugu au biashara haramu ya binadamu, WhatsApp itawapiga marufuku wanajumuiya au wasimamizi binafsi, itafuta Jumuiya, au itawapiga marufuku wanajumuiya wote. Ili kuchukua hatua inayofaa, tutatumia taarifa zote zinazopatikana ambazo hazijasimbwa kwa njia fiche, ikijumuisha jina la Jumuiya, maelezo na ripoti za watumiaji.
WhatsApp itaendelea kuboresha Jumuiya katika miezi na miaka ijayo na kama kawaida tutaendelea kusikiliza maoni ya watumiaji kuhusu jinsi tunavyoweza kuwasaidia watu kuwasiliana kwa faragha na kwa njia salama.
Je, hii ilikusaidia?
Ndiyo
La